Thursday, April 24, 2014

Na Ezekiel Kamanga.
UONGOZI wa Hospitali ya Rufaa ya Mbeya kupitia kitengo cha Ustawi wa jamii  umemtafutia kituo cha kulelea watoto wa mitaani cha Nuru Ophans Centre Mama aliyejifungua mapacha wanne na kubakia wawili baada ya kuugua Nimonia kwa ajili ya uangalizi wa karibu.
 
Hatua hiyo imekuja baada ya uongozi wa Hospitali hiyo kumfuata mama mwenye watoto hao Aida Nakawala(25) pamoja na mapacha wake waliobaki kutoka kijijini kwao Chiwanda Wilaya ya Momba mkoani hapa na kuwalaza hospitalini hapo kwa uangalizi wa karibu kwa muda wa zaidi ya wiki moja.
 
Aidha baada ya afya za watoto hao  kuimarika kwa kiwango kikubwa pia Uongozi wa Hospitali hiyo imemtafutia hifadhi katika kituo cha kulelea watoto wa mitaani cha Nuru kilichopo Uyole jijini Mbeya kwa ajili ya uangalizi wa karibu kutoka kwa wauguzi na maafisa wa ustawi wa Jamii kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mbeya.
 
Akizungumza na waandishi wa habari wakati akiwakabidhi watoto hao pamoja na mama yao kwenye uongozi wa kituo cha Nuru Orphans centre, Katibu wa Hospitali ya Rufaa ya Mbeya, Aisha Mtanda, alisema wameguswa na mazingira anayoishi mama huyo na kuamua kumpa uangalizi kwa miezi sita zaidi.
 
Alisema jukumu hilo halipaswi kufanywa na Hospitali kwa kuwa tayari  walikuwa wamemaliza jukumu lao la kumhudumia alipokuwa ana matatizo lakini wamelazimika kubeba jukumu hilo baada ya kuguswa na mazingira na hali ya makazi ya familia hiyo.
 
Alisema Hospitali imekubaliana na uongozi wa Kituo cha Nuru kwamba apewe hifadhi mama huyo na watoto wake ili apate uangalizi wa karibu ikiwa na lengo la kunusuru maisha ya watoto waliobaki kutokana na wengine kupoteza maisha kiuzembe kwa ugonjwa wa Nimonia.
 
Aliongeza kuwa Hali ya hewa ya Mkoa wa Mbeya kwa siku zijazo kunakuwa na baridi kali sana hivyo watoto wasipokuwa kwenye uangalizi wa karibu wanaweza kupatwa na ugonjwa wa Nimonia tena kwa kukosa matunzo kama ya awali.
 
Kwa upande wake, Meneja wa Kituo cha Nuru, Amanda Fihavango alisema alikubali jukumu la kuwapokea watoto hao pamoja na mama yao kutokana na kuguswa na hali iliyowakuta ya kupotea kwa watoto wawili kati ya wanne.
 
Aliongeza kuwa ingawa anakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo za kiuchumi atajitahidi kwahudumia kadri ya uwezo wake na kuomba wasamaria wema watakaoguswa na jambo hilo kujitolea kwa hali na mali kufanikisha kuokoa uhai wa watoto hao pamoja na wengine anaowalea.
 
Alisema kituo chake hupokea watoto waliookotwa baada ya kutupwa na wazazi wao au mama zao kufariki mara baada ya kutoka kujifungua ambao hupelekwa na Serikali kupitia Ustawi wa Jamii ingawa haichangii fedha zozote baada ya kuwapeleka.
 
Mtu yoyote mwenye kuguswa anaweza kuwasilisha mchango wake kituoni hapo au kuwasiliana na Meneja wa Kituo cha Nuru kupitia namba za Simu  0754 043004 kwa ajili ya kusaidia watoto hao pamoja na mama yao kuishi hapo kwa muda wa miezi sita.
 

Askari wafikishwa mahakamani Mbeya

Na Venance Matinya, Mbeya.
ASKARI wa Jeshi la Polisi na raia mmoja wamefikishwa mbele ya Mahakama ya Wilaya ya Mbeya wakituhumiwa kwa makosa mawili ambayo ni kula njama za kutenda kosa pamoja na wizi wa mtoto.
 
Watuhumiwa hao ni pamoja na Mshtakiwa wa kwanza aliyekuwa Ditektivu Constebo wa Polisi mwenye namba WP 5367  Prisca Isaya (35) mwenyeji wa Ilala Dar es salaam ambaye hata hivyo alivuliwa vyeo na kufukuzwa kazi kabla ya kupandishwa Mahakamani  na Salehe Mwangosi (28) mkazi wa Njisi wilayani Kyela Mkoa wa Mbeya.
 
Akisoma mashtaka yanayowakabili Mwendesha mashtaka wa Serikali, Juliana William, mbele ya Hakimu wa Wilaya ya Mbeya, Maria Batulaine, alisema watuhumiwa wote kwa pamoja wanakabiliwa na makosa mawili waliyoyatenda Aprili 4, Mwaka huu.
 
Alisema kosa la kwanza ni kula njama kwa nia ya kutenda kosa la kuiba mtoto kinyume cha kifungu cha 384 (16) cha kanuni ya adhabu kilichofanyiwa marejeo mwaka 2002 walilofanya Aprili 4, Mwaka huu katika eneo la Songwe wilayani Kyela.
 
Alitaja kosa la pili kuwa ni Wizi wa mtoto  kinyume cha kifungu cha 169 (1) (a) sura ya 16 ya kanuni ya adhabu kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
 
Mwendesha mashtaka huyo aliiambia Mahakama kuwa washtakiwa wote kwa pamoja mnamo Aprili 6, Mwaka huu katika eneo la Zahanati ya Njisi Wilaya ya Kyela Mkoani hapa kwa maksudi waliiba mtoto mwenye umri wa siku saba kutoka kwa  mama yake mzazi Mboka Mwakikagile.
 
Washtakiwa wote kwa pamoja walikana kuhusika na tukio hilo ambapo upande wa mashtaka ulidai upelelezi wa shauri hilo umekamilika na upo tayari kuwaleta mashahidi wake kwa ajili ya kuendelea na usilizwaji wa kesi.
 
Kwa upande wake Hakimu aliahirisha kesi hadi Mei 6, Mwaka huu na kwamba dhamana kwa washtakiwa iko wazi kama watakidhi vigezo ambavyo ni kila mmoja kuwa na wadhamini wawili wenye mali zisizo hamishika zenye thamani ya shilingi Milioni 5, barua ya mtendaji na barua kutoka kwa mwajiri kwa ajili ya mshtakiwa wa kwanza.
 
Hata hivyo walishindwa kuwa na wadhamini waliokidhi vigezo vya mahakama na kuamliwa kurudishwa rumande hadi Mei 6, Mwaka huu kesi itakapo kuja kwa ajili ya kusikilizwa.

Wednesday, April 23, 2014

Sir Alex Ferguson
Duru zinasema kuwa Sir Alex Ferguson,atahusika katika kuteua meneja atakayechukua mahala pa David Moyes.

Moyes, aliyeteuliwa na Ferguson kumrithi mwaka jana, alifutwa kazi baada ya kuhudumu kwa miezi kumi pekee.

Kuanzia sasa Ferguson atahusika katika uteuzi huo pamoja na wanachama wote wa bodi.

Wakati wa miaka yake 26 kwenye usukani wa meneja wa klabu hiyo, Ferguson aliweza kushinda mataji 38 ikiwemo 13 ya ligi ya mabingwa mwaka 1999 na mwaka 2008.

Chini ya uongozi wa Moyes, United wameshindwa katika mechi sita nyumbani , wamepata kichapo katika michuano ya FA na kuhindwa katika michuano ya kombe la Capital One katika nusu fainali.

Man U wanashikilia nafasi ya saba wakiwa wamesalia na mechi nne katika ligi kuu ya Uingereza.


Rekodi ya David Moyes

Moyes ameonekana kutofanya vyema na ndio maana akatimuliwa

David Moyes amefutwa kazi na Manchester United baada tu ya miezi kumi kama meneja wa klabu hiyo.

Rekodi ya Moyes sio kitu ikilinganishwa na miaka 26 ya usukuni wa Alex Ferguson katika klabu hiyo.
Anaaga klabu hiyo ikiwa imeshikilia nafasi ya saba. Pia itakosa fursa ya kucheza katika ligi ya mabingwa wa Ulaya kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1995 na pia wako katika hatari ya kukosa kushiriki michuano ya bara ulaya tangu mwaka 1990.

Mameneja waliowahi kushikilia wadhifa huo kwa muda mfupi sana ni pamoja na Sir Matt Busby aliyekuwa meneja wa klabu hiyo kati ya mwaka 1945-1969 aliyerejea tu kama swala la dharura mwaka 1970, na meneja mwingine Jimmy Murphy aliyeshikilia nafasi ya Sir Matt baada ya ajali ya ndege ya Munich mwaka 1958.

Moyes ni kocha wa tatu katika historia ya klabu hiyo kuingoza kwa muda mfupi zaidi.

Kadhalika Moyes alikuwa kocha wa Everton kwa miaka kumi kwa kuipa ukakasi na kuirejesha katika nafasi nzuri kwenye ligi kuu.

Moyes alitarajiwa kuendeleza ufanisi wa klabu hiyo lakini hiyo ilikuwa changamoto kubwa sana kwake na ndio sababu kubwa ya yeye kutimuliwa.

Chanzo BBC

Tuesday, April 22, 2014

Breaking News... Ajali ya magari ya mizigo yaua Mbeya

Ajali ya magari ya magari matatu ya mizigi imetokea Vwawa Wilaya Mbozi mkoani Mbeya imesadikika dereva wa gari aina ya tipa amefikwa na mauti papo hapo na wengine kujeruhiwa vibaya.

Kwa habari kamili usikose kutembelea mtandao huu.

Friday, April 11, 2014


Klabu ya Chelsea huenda ikafaidika na kiasi cha paund million 6, endapo itapangwa na klabu ya Atletico Madrid katika hatua ya nusu fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya.

Chelsea wanajipanga kupokea kitita hicho cha pesa, kama wataangukia mkononi mwa Atletico Madrid katika hatua hiyo kufuatia kifungu kilichopo kwenye makubaliano ya klabu hizo mbili wakati The blues wakikubali kumpeleka kwa mkopo mlinda mlango kutoka nchini Ubelgiji Thibaut Courtois huko Estadio Vicente Calderón.

Imeripotiwa kwamba katika makubaliano hayo, kuna kifungu ambacho kipo kwenye mkataba wa mlinda mlango huyo mwenye umri wa miaka 21 ambacho kinaishurutisha klabu ya Atletico Madrid kutomtumia Thibaut Courtois endapo itatokea wanakutana na Chelsea kwenye michuano ya kimataifa.

Kifungu hicho kimeendelea kusisitiza kwamba endapo Atletico itawalazimu kumtumia kipa huyo itawagharimu kuwalipa Chelsea kiasi cha paund million tatu kwa kila mchezo watakaomtumia Thibaut Courtois.

Kama klabu hizo zitapangwa kukutana katika mchezo wa hatua ya nusu fainali, na Atletico Madrid wakafanya maamuzi ya kumchezesha mlinda mlango huyo katika mchezo wa nyumbani na ugenini, itawalazimu kuwalipa Chelsea paund million 6.

Hata hivyo kitendawili cha Atletico Madrid kupangwa na Chelsea katika mchezo wa hatua ya nusu fainali, kitateguliwa kesho mara baada ya upangaji wa michezo ya hatua ya nusu fainali, ambapo hafla yake itafanyika mijini Nyon nchini Uswiz.

Atletico Madrid wamefanikiwa kutinga katika hatua ya nusu fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya, baada ya kuifunga FC Barcelona bao moja kwa sifuri katika mchezo uliochezwa usiku wa kuamkia hii leo huko jijini Madrid.

Baada ya ushindi huo klabu hiyo Estadio Vicente Calderón, imesonga mbele kwa jumla ya mabao mawili kwa moja na kuungana na FC Bayern Munich, Chelsea pamoja na Real Madrid ambazo zimetinga kwenye hatua ya nusu fainali.

Thursday, April 10, 2014


Mwenyekiti wa Mtaa wa Mapelele kata ya Ilemi, jijini Mbeya anashtumiwa kwa kutafuna pesa shilingi 1,300,000 zilizochangwa na wananchi kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya serikali ya mtaa.

Bofya hapa kusikiliza habari kamili inayoletwa kwako na mwandishi wetu Greyson Salufu Chatanda.


Kumekucha ndani ya Klabu ya Simba Sc.Katibu Mkuu wa Klabu ya Simba Sc, Ezekiel Kamwaga.
****
Kamati ya uchaguzi ya klabu ya Simba leo inatarajia kukutana chini ya mwenyekiti wake Damas Ndumbaro huku ajenda kuu ikatayo kiongoza kikosi cha kamkati hiyo ni mustakabali wa uchaguzi wa viongozi wa klabu ya Simba kwa kipindi cha miaka minne ijayo.

Katibu mkuu wa klabu ya Simba Ezekiel Kamwaga amesema kikao hicho cha kamati ya uchaguzi kitakua ni cha kwanza kwa kamati hiyo na anaamini jibu la mustakabali wa uchaguzi lipatikana kwa nia sahihi kutokana na kila mjumbe kutambua umuhimu wa upatikanaji wa viongozi wapya kwa kutimia katiba.


Katika hatua nyingine katibu mkuu wa klabu ya Simba Ezekiel amezungumzia maendeleo ya marekebisho ya katiba waliyoyafanya katika mkutano mkuu wa wanachama uliofanyika jijini Dar es salaam mwezi March.

Kamwaga amesema mara baada ya kukamilika kwa zoezi la marekebisho ya katiba walifanya utaratibu wa kuiwasilisha katiba yao kwenye ofisi za shirikisho la soka nchini TFF na kasha wakaendelea na hatua nyingine ya kuifikisha kwa msajili kwa lengo la kukamilishwa kwa mchakato huo.

BARCELONA, MAN U ZAFUNGASHIWA VIRAGO UEFA.

MANCHESTER United ya England imeaga Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kufungwa mabao 3-1 na wenyeji Bayern Munich Uwanja wa Allianz-Arena mjini Munich, Ujerumani usiku huu.

Hiyo inamaanisha United imeaga kwa kipigo cha jumla ya mabao 4-2, baada ya awali kulazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 Uwanja wa Old Trafford mjini Manchester.

United leo ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 57, mfungaji beki wake Mfaransa, Patrice Evra aliyefumua shuti kali kwa guu la kushoto baada ya kupokea pasi ya Antonio Valencia.

Sekunde 22 baadaye Mcroatia Mario Mandzukic akaisawazishia Bayern akitumia fursa ya wachezaji wa United kuzubaa kwa furaha ya bao, wakidhani  biashara imekwisha na kumbe mpira ni hadi filimbi ya mwisho.

Bao hilo liliwaondoa mchezoni United na kuanza kufanya madudu, hali ambayo iliwapa fursa mabingwa hao wa Ulaya kupata mabao mawili zaidi.

Tomas Muller alifunga la pili dakika ya 68 pasi ya Arjen Robben ambaye alikuwa mwiba mchungu kwa Mashetani hao Wekundu usiku huu. 

Arjen Robben akafunga mwenyewe bao la tatu kwa shuti la mbali dakika ya 76 na kuzima kabisa ndoto za kocha David Moyes kufanya maajabu kwenye michuano hiyo ya Ulaya.

Katika mchezo mwingine, Barcelona imefungishwa virago na Atletico Madrid, zote za Hispania baada ya kufungwa bao 1-0 Uwanja wa Vicente Calderon mjini Madrid, Hispania.

Hiyo inamaanisha Barca imeaga kwa kipigo cha jumla cha mabao 2-1 baada ya awali kulazimishwa sare ya 1-1 Uwanja wa Camp Nou, Barcelona.  

Bao lililoizamisha Barca leo limefungwa na Jorge Resurrecion Merodio Koke dakika ya tano akimalizia pasi ya Adrian.

Bayern na Atletico zinaungana na Chelsea ya England iliyoitoa PSG ya Ufaransa na Real Madrid ya Hispania iliyoing’oa Borrussia Dortmund jana kutinga Nusu Fainali, ambayo droo yake itapangwa Ijumaa.   

Saturday, April 5, 2014


Makodakta wa magari ya abiria yaendayo Mji mdogo wa Mbalizi wilaya ya Mbeya Vijijini wameshtumiwa kwa kusababisha ajali zisizo za lazima kutokana na kuendesha vyombo vya moto bila leseni.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti mmoja wa abiria wamesema tatizo hilo limekuwa sugu akama anavyosimulia kisa kimoja wapo kilichowahi kutokea eneo la stendi ya Kabwe.

 HABARI ILIYOANDIKWA NA GREYSON SALUFU INASOMA KWAKO...

Abiria wa magari ya usafirishaji yaendayo pembezoni mwa Jiji la Mbeya wamelalamikia tabia ya madereva hao kuzungumza na simu pindi waendeshapo magari hayo.

Kwa habari kamili sikiliza hapa chini.


Kushoto Afisa tarafa Aaron Sote akipokea funguo toka kwa mtendaji Anton Ndisa 

Afisa Kilimo wilaya Marselin Mlelwa atitoa takwimu  za mgao wa mbolea iliyotolewa Octoba 10 mwaka jana kwa kijiji hicho baada ya kupitishwa na Kamati ya Mbolea ya Wilaya ambayo mwenyekiti wake ni Mkuu wa Wilaya.

Wananchi wakifuatilia mkutano huo kwa makini


Saimoni Kasebele moja kati ya wajumbe kamati ya mbolea ambayo haikufanya kazi kijijini

Moja kati ya wananchi ambao waliwekwa mahabusu na mtendaji baada ya kufuatilia mgao wa mbolea


Wajumbe waliotimuliwa


Mbolea inayosadikiwa kuibwa Kwa picha zaidi tazama hapa PICHA ZAIDI

Wananchi wa kijiji cha Iwiji Kata ya Iwiji wilaya ya Mbeya wamemtimua Mtendaji wa Kijiji hicho ambaye pia ni Kaimu Mtendaji Kata aliyefahamika kwa jina la Anthon Ndisa kwa tuhuma za ubadhilifu wa Mbolea za ruzuku mifuko 189 iliyotolewa na serikali kwa kipindi cha msimu wa 2013/2014.

Hatua hiyo imechukuliwa na wananchi hao katika mkutatano wa hadhara uliofanyika kijijni hapo ambapo Afisa Kilimo wilaya Marselin Mlelwa atitoa takwimu  za mgao wa mbolea iliyotolewa Octoba 10 mwaka jana kwa kijiji hicho baada ya kupitishwa na Kamati ya Mbolea ya Wilaya ambayo mwenyekiti wake ni Mkuu wa Wilaya.

Afisa Tarafa ya Isangati Aaron Sote ambaye alimwakilisha Mkuu wa Wilaya ndiye alisimamia mkutano huo amesema kuwa Afisa kilimo ndiye mwenye jukumu la kutoa taarifa ya mgao wa mbolea kama kamati ilivyopitisha.

Baada ya kufunguliwa mkutano  na Mwenyekiti wa kijiji Patson Ngao Afisa Tarafa alimkaribisha Afisa Kilimo kusoma jinsi mgao wa mbolea ulivyokwenda ambapo alisema Kitongoji cha Mabula kilipata mbolea ya Dap mifuko 20 Urea 20, Kitongoji cha Iwiji Dap mifuko 8 Urea 20,Kitongoji cha Soweto mifuko 6 Dap na Urea mifuko 16.

Kitongoji cha Magole kilipata Dap mifuko 6 na Urea mifuko 16,Kitongojo cha Mtukula Dap mifuko 6 na Urea mifuko 16 wakati Kitongoji cha Ntinga kilipata Dap mifuko 8 na Urea mifuko 20 wakati Kitongoji cha Vimetu kikipata Dap mifuko 7 na Urea mifuko 20.

Katika mgao huo kulikuwa na upungufu wa mifuko 50 ya Dap na Urea mifuko 36 ambayo wakulima hawajapatiwa na kwamba ikifika wananchi wagawiwe ili kukamilisha idadi ya mifuko 189 kwani hivi sasa mifuko iliyogawiwa ni mifuko 139 tu.

Baada ya kusomwa taarifa hiyo wananchi walitaharuki wakidai kuwa hesabu hizo zimetengezwa na Mtendaji Anthon Ndisa kwa manufaa yake kwani wananchi hawajapata mbolea hiyo licha ya kutoa taarifa kwa uongozi wa Wilaya kupitia Afisa Pembejeo Lupakisyo Masuba.

Kutokana na kutoridhishwa na taarifa hiyo na kwamba wananchi wamehujumiwa na uongozi wa kijiji kupitia viongozi wa vitongoji ambao walikiri kupokea mbolea hiyo na kuigawa wakati kuna kamati mbolea ya kijiji ambayo ndiyo ilikuwa na jukumu la kugawa ambapo uongozi wa kijiji ukidai kamati hiyo ilivunjwa.

Mmoja wa wajumbe wa Kamati ya pembejeo Simon Kasebele amesema kuwa kati iliyokuwa na wajumbe sita ambao ni Mwenyekit Venance Lwinga,Lucia Mose,Sara Kasalama,Patson Kayelewe na Eva Makanika haikufanya kazi kutokana na agizo la Mtendaji aliyedai kuwa kamati imevunjwa wakati siyo kweli bali ilikuwa ni njama za kuwahujumu wananchi kwa manufaa yao.

Baada ya majadiliano marefu wananchi waliamua kuirudisha Kamati ya Mbolea huku wakimtaka Mtendaji kuondolewa haraka ili kuepusha ufujwaji wa mali za kijiji na kuwatimua wenyeviti wote wa vitongoji na kumwacha Mwenyekiti wa kijiji pekee Patson Ngao wakidai hahusiki na ubadhilifu kwani alizungukwa na Mtendaji kupitia wenyeviti wa vitongoji.

Kwa upande wake Afisa Kilimo Marselin Mlelwa amesema taarifa ataifikisha kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ili kutoa maamuzi kwa vile Mtendaji ni Mwajiriwa hivyo lazima taratibu za utumishi lazima zifuatwe.

Ili kuhakikisha hakuna nyaraka zozote zinachukuliwa Ofisi Mwenyekiti na Kamati ya Mbolea watafanyia shughuli zao katika ghala la Kijiji wakati Mtendaji aliagizwa kubaki na funguo hadi hapo Halmashauri itakapotoa taarifa zake baada ya ukaguzi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Upendo Sanga amekiri kupokea taafa za malamiko ya wananchi wa Iwiji na kuwataka kuwa na subira kwani serikali ina utaratibu wake ambao lazima ufuatwe pindi mtumishi anapotuhumiwa kwa jambo lolote ikiwa na pamoja na kuunda Tume ya Uchunguzi na Wakaguzi ili kupata Ushahidi.

Uchunguzi uliofanywa baada wananchi kulalamikia utaratibu uliotumika kugawa mbolea hiyo Mtendaji wa Kijiji alirejesha mifuko 50 ya Dap ambayo imehifadhiwa kwa mmoja wa Mawakala kijijini hapo ili kuficha ushahidi na kuonekana mbolea hiyo ilikuwepo wakat ukweli ni kwamba mbolea hiyo tangu itolewe mwezi Octoba wananchi hatanufaika nayo kwa kuwa msimu wa kilimo umepita na kijiji kukabiliwa na hatari ya njaa.

Mbali ya tuhuma ya Mbolea Mtendaji anatuhumiwa kufuja fedha za serikali na michango ya wananchi kwa ajili ya kituo cha Afya hivyo wamemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri anapofanya uchunguzi wa Mbolea afanye ukaguzi pia mradi wa Kituo cha Afya na kama ikibainika Mtendaji na Halmashauri ya Kijiji wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.

Na Ezekiel Kamanga

Tuesday, April 1, 2014

MAHAKAMA ya wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya jana(Machi 31) imemhukumu
kutumikia kifungo cha jumla ya miaka 65 jela mkazi wa mtaa wa Uhamila
katika mji mdogo wa Rujewa kutokana na makosa matatu tofauti
yaliyotokana na kumpa ujauzito mwanaye wa kumzaa.

Mshitakiwa aliyehukumiwa kifungo hicho ni Benjamin Muyinga(48) ambapo
mashitaka aliyokuwa akikabiliwa nayo mahakamani hapo ni Kufanya
mapenzi na mtoto wake,kubaka mtoto wake na la tatu ni kumpa mamba
mwanafunzi.

Awali ilielezwa mahakamani hapo na mwendesha mashitaka wa jeshi la
polisi Mazoya Luchagula,mbele ya hakimu mfawidhi Kinabo Minja kuwa
mnamo Oktoba 18 mwaka 2013 mwanafunzi(jina linahifadhiwa) aliyekuwa na
umri wa miaka 14 alikuwa mjamzito.

Luchagula alisema walimu wa shule hiyo ndiyo walitilia shaka suala la
mwanafunzi huyo aliyekuwa darasa la tano katika shule ya msingi Ibara
iliyopo Rujewa kuwa alikuwa na ujauzito na ndipo alipelekwa hospitali
na kwenda kukutwa akiwa na mamba ya miezi minne.

Alisema baada ya kuhojiwa mwanafunzi huyo alisema kuwa ujauuzito
ulikuwa wa baba yake mzazi waliyekuwa wakiishi naye wawili nyumbani
kwao kufuatia baba huyo kutengana na aliyekuwa mkewe ambaye hivi sasa
anaishi jijini Mbeya.

Alisema mwanafunzi huyo alibainisha namna alivyokuwa akiishi na baba
yake baada ya wazazi wake kutengana na ndipo baba yake akamgeuza
mwanaye huo kuwa mkewe ambapo alikuwa akilala naye na kufanya naye
mapenzi hadi ilipobainika kuwa na ujauzito huo.

Kutokana na kitendo kilichofanywa na mzazi huyo kutokubalika katika
jamii ya watanzania,mwendesha mashitaka aliiomba mahakama hiyo kutoa
adhabu kali kwa mshitakiwa ili kumpa fundisho yeye na wazazi wengine
wenye tamaa zenye kusababisha ukatili dhidi ya watoto wao.

Kufuatia kuridhishwa na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo,hakimu
mfawidhi Minja alimhukumu mzazi huyo katili kutumikia kifungo cha
jumla ya miaka 65 jela kwa makosa hayo matatu kitakachotekelezwa kwa
wakati mmoja ili iwe fundisho kwa wazazi wenye tabia hizo.

Hakimu huyo alimhukumu mshitakiwa kutumikia jela miaka 30 kwa kosa la
kufanya mapenzi na mtoto wake,miaka 30 mingine kwa kubaka mtoto wake
na miaka mitano jela kwa kumpa mamba mwanafunzi.

Saturday, March 29, 2014

Epuka Zuia Wizi Wa Mtandao
Jamii imetahadharishwa kuwa makini na vitendo vya wizi na utapeli vinavyofanywa mitandaoni na imetakiwa kutoa taarifa Polisi pindi wanapowabaini kuhusika na vitendo hivyo ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.

 KWA HABARI KAMILI INALETWA KWAKO NA GREYSON SALUFU CHATANDA...... Bofya hapa chini kwa habari kamili.


KARIBU KWA MAONI YAKO...

Monday, March 24, 2014

Tuzo ya mwalimu bora duniani yazinduliwaMwenyekiti wa Wakfu huo Rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton.

Baadhi ya walimu jijini Mbeya  wameipokea kwa mtazamo tofauti  juu ya kuzinduliwa kwa tuzo ya mwalimu duniani, atakaye thibitisha kuwa mchango wake kwa jamii umekuwa bora zaidi na kujishindia shilingi bilioni 1 na milioni 650.KWA HABARI KAMILI INALETWA KWAKO NA GREYSON SALUFU...... Bofya hapa chini kwa habari kamili.

Malaysia:Ndege ilianguka baharini


Waziri mkuu wa Malaysia Najib Razak.


Shirika la ndege la Malaysia limewaambia jamaa na familia za abiria waliokuwa wanasafiri kwa ndege iliyotoweka MH370 kwamba ndege hiyo imepotea na kwamba hakuna manusura.

Tangazo hilo limetolewa kwa familia hizo kwa njia ya ujumbe wa simu ya mkononi , ambao BBC iliweza kuuona.
Ndege ya Malaysia MH320 ilitoweka ikiwa na abiria 239 baada ya kuruka kutoka uwanja wa ndege wa Kuala Lumpur tarehe 8 mwezi huu.

Aidha tangazo hilo limekuja huku juhudi za kutafuta mabaki ya ndege hiyo Kusini mwa Bara Hindi zikimalizika kwa siku ya tano bila mafaniko.

Waziri mkuu wa Malaysia amesema kuwa ndege hiyo ilianguka Kusini mwa Bahari Hindi, bila ya manusura wowote.

Aliambia waandishi wa bahari kuwa udadisi uliofanyiwa data ya Satelite kutoka Uingereza ndio umewathibitishia kwamba ndege hiyo ilimalizia safari yake Magharibi mwa mji wa Perth mbali na eneo lolote la kutua.

Ameomba vyombo vya habari kuheshimu familia za watu waliokuwa ndani ya ndege hiyo, akisema kuwa anasikitishwa sana kwani kipindi chote walichosubiri taarifa njema , mwishowe imekuja kuwa taarifa mbaya hata zaidi.

Ndege ya Malaysia MH-370, ilipoteza mawasiliano wiki mbili zilizopita na meli za nchi mbali mbali pamoja na ndege zimekuwa zikitafuta angalau mabaki ya ndege hiyo bila ya kupata chochote.

Chanzo - BBC

Mtoto aliyefahamika kwa jina la Eva Mathias Kankolwe mwenye umri wa miaka 10 mkazi wa Kata ya Kiwira wilayani Rungwe amekufa maji baada ya kutereza katika kivuko cha mto Kiwira wakati akitokea kuokota kuni.

MWANDISHI WETU GREYSON SALUFU AMETUANDALIA TAARIFA IFUATAYO..... Bofya hapo chini kusikiliza habari kamili.

Recent Posts